MH PHILEMON NDESAMBURO
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Philemon Ndesamburo, ametangaza kung’atuka kugombea nafasi hiyo, katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Ndesamburo alitangaza uamuzi huo jana baada ya kuongoza Jimbo hilo kwa vipindi vitatu mfululizo.
Mbunge huyo anatarajiwa kukabidhi mikoba yake kwa Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Japhary Michael.
Ndesamburo alitangaza uamuzi huo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Manyema kata ya Bondeni, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, ambapo alisema amefikia uamuzi huo kutokana na chama hicho kuwa cha demokrasia.
Alisema ameamua kung’atuka na kukabidhi mikoba yake kwa Japhary Michael, kwa sababu ni mtu safi na anaamini anaweza kurithi viatu vyake na kuliongoza jimbo la Moshi kwa uaminifu na kuwaletea wananchi
maendeleo.
“Napenda kutangaza rasmi kung’atuka ubunge wangu, lakini nitawapatia mtu safi ambaye nitamkabidhi kwenu leo hii kushika mikoba yangu,kwani ni mtu mzuri, si mwizi, si fisadi; na mimi natumia demokrasia;na nitampigia kampeni kwa nguvu zangu zote," alisema Ndesamburo huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Ndesamburo alisema amefanya hivyo ili kuondoa makundi ndani ya chama hicho; na kujenga umoja, ikiwa ni hatua mojawapo za kuhakikisha chama hicho kinaendelea kushinda katika jimbo hilo na kuongoza manispaa ya Moshi.
Alisema atatumia nguvu zake zote na kufanya jitihada ili kuhakikisha Japhary anashinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu na kutangazwa kuwa Mbunge
wa jimbo la Moshi Mjini.
Alisema Japhary katika uongozi wake kama Meya wa Manispaa ya Moshi,
ameweza kusimamia baraza la madiwani ambalo linaongozwa na CHADEMA na kudhibiti mianya ya rushwa na kuongeza mapato ya Halmashauri.
“Katika uongozi wa Japhary, Manispaa imekuwa na mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kujengwa kwa miundombinu ya barabara, wafanyabiashara wadogo kupatiwa maeneo ya kufanyia biashara na kuondokana na kero na usumbufu waliokuwa wakiupata hapo awali.
Ni mtu makini na anaweza kurithi vyema viatu vyangu na kuliongoza jimbo
hili,” alisema.
Ndesamburo alitumia pia nafasi hiyo kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi, kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, hatua ambayo itawawezesha kupata fursa ya kutimiza haki yao ya msingi
kisheria ya kupiga kura.
Alisema hatua ya wananchi kujiandikisha kwa wingi pia itasaidia kumwezesha Japhary kuibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu pamoja na wagombea wa udiwani wa chama hicho watakaosimama kuwania nafasi hizo.
Japhary baada ya kukabidhiwa mikoba na Ndesamburo,alishuka kwenye jukwaa na kwenda kukaa huku akibubujikwa na machozi.
No comments:
Post a Comment