Wednesday, February 11, 2015

WAPANGAJI JENGO LA TRENI MJI MKONGWE WATAKIWA KUHAMA JENGO HILO


14
Na Abdulla Ali, Maelezo-Zanzibar                                             
SERIKALI haitoridhia kuwabakisha Wapangaji na Wafanyabiashara katika jengo la Treni ili kuepusha maafa na kuokoa maisha ya Wananchi na mali zao.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Zanzibar Mhe. Ramadhan Abdulla Shaaban wakati wa mkutano wa mzungumzo ya pamoja kati ya Wapangaji na  Wafanyabiashara wanaolitumia jengo hilo na Serikali uliofanyika katika ofisi ya Mamlaka ya Mji Mkongwe iliopo Forodhani Mjini Zanzibar.
Waziri huyo amesema kuhamishwa kwa Wakaazi na Wafanyabiashara katika jingo hilo sio jambo la mjadala kama wanavyotaka wao bali ni wajibu wao kufuata maagizo ya serikali ili kuepukana na vifo visivyo vya lazima na hasara za mali zao pindi jengo hilo litakapo poromoka na kupelekea kuitupia lawama serikali pale majanga yatakapotokezea.
“Hili si jambo la majadiliano kama mnavyotaka nyinyi”, alieleza Waziri Ramadhan.
Ametanabahisha kuwa serikali imeshachukua hatua mbalimbali za kulijenga tena jengo hilo ikiwemo kutafuta mafundi, wahandisi pamoja na vifaa vya ujenzi na inategemewa hivi karibuni kuanza rasmi kwa ujenzi huo.
Aidha waziri ramadhan amewataka Wapangaji na Wafanyabiashara hao kutokaidi agizo la Serikali kwa usalama wa mali na maisha yao kwani jengo hilo linaonekana halitoweza kuhimili mvua za Masika zinazotarajiwa kuanza mwezi machi mwaka huu na badala yake linaweza kuporomoka kutokana na mvua hizo.
Jengo la Treni liliopo Darajani Mjini Zanzibar lina wakaazi 57 wakiwemo Wapangajia na Wafanyabiashara ambapo kwa sasa hali yake hairizishi baada ya kupasukapasuka na kutishia usalama wa maisha ya watu wanaoishi humo pamoja na wapita njia.

No comments:

Post a Comment