Friday, February 13, 2015

IFAHAMU MAANA KAMILI YA VALENTINE'S DAY NA WAWEZA VIPI KUISHEREHEKEA..


VALENTINE'S Day ama kwa Kiswahili Siku ya Wapendanao, huadhimishwa kila Februari 14 ambapo kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, siku hiyo inazidi kuwa maarufu na kuadhimishwa kwa shangwe ingawa wengi hushindwa kuelewa hasa maana yake.
Ukiwauliza wengi nini hasa maana ya Valentines Day, ni wachache wanaoweza kukueleza kwa ufasaha maana yake na kwa sababu hiyo, wengi wanakuwa na kawaida ya kuiadhimisha siku hiyo kwa mazoea tu, huku wakifanya mambo ambayo hayafai mbele ya jamii.
HISTORIA YA SIKU YA WAPENDANAO
Mtakatifu Valentine ndiye hasa muasisi wa Siku ya Wapendao ambapo karne nyingi zilizopita, katika utawala wa Warumi, alikuwa akipita kwenye magereza ya wafungwa wa kivita na kambi za wanajeshi, akiwahubiria watu habari za kuwa na upendo kati yao.
Mtakatifu Valentine hakuishia hapo, alifanya pia kazi ya kuwafungisha ndoa kwa siri wanajeshi wa Kirumi ambao hawakuwa wakiruhusiwa kuoana wawapo kambini. Kazi hiyo ya kuwafungisha ndoa na kuhubiri upendo, ilisababisha Mtakatifu Valentine akamatwe na kutupwa gerezani kwa kuvunja sheria za utawala wa Kirumi.
Akiwa gerezani, Mtakatifu Valentine aliendelea na kazi yake ya kuwahubiria wafungwa wenzake upendo, kuwasaidia waliokuwa wagonjwa kwa kuwaponya, kuwafungisha ndoa wanajeshi kwa siri na kuendeleza huduma za kiroho zikiwemo kuwaombea watu wenye matatizo mbalimbali.
Kesi yake iliendelea kuunguruma, akishtakiwa kwa kosa la kuwafungisha ndoa wanajeshi wa Kirumi, jambo ambalo lilikuwa ni kinyume na sheria za kipindi hicho, mwisho akahukumiwa adhabu ya kifo.Akiwa anaendelea kusubiri siku yake ya kunyongwa, mtoto wa mkuu wa gereza alilokuwa amefungwa aitwaye Asterius, alipatwa na maradhi ya ajabu ambayo yalisababisha akaribie kukata roho.
Mtakatifu huyo aliposikia habari hizo, aliomba kwenda kuonana naye ambapo alimponya maradhi yaliyokuwa yanamsumbua. Habari za tukio hilo la kipekee, lililodhihirisha upendo wa dhati, zilisambaa kwa kasi ndani na nje ya gereza.
Siku chache kabla Mtakatifu Valentine hajanyongwa, alimuandikia barua ya kumuaga binti huyo wa mkuu wa gereza, chini kabisa akaandika maneno ‘Your Valentine’, akaambatanisha na ua waridi jekundu.
Hata aliponyongwa na kufa, wafuasi wake waliokuwa wakiyakubali mafundisho yake, waliendelea kuiadhimisha siku aliyonyongwa, Februari 14 kwa kupeana kadi na barua zenye maneno ‘Your Valentine’ au ‘To My Valentine’ kudhihirisha upendo waliokuwa nao kwa wahusika.
TAFSIRI SAHIHI
Kwa kuitazama historia hiyo fupi, tunajifunza kuwa kumbe Valentines Day siyo siku ya kufanya ngono hovyo, kuanzisha uhusiano wa kimapenzi, kulewa na kufanya kufuru nyingine kama hizo bali ni siku ya kuoneshana upendo, kupeana zawadi zikiwemo kadi nzuri, maua na chocolate.
Na unayemfanyia hivyo, siyo lazima awe mpenzi wako, anaweza kuwa mama yako, baba yako, rafiki yako, mwanao au mtu yeyote unayetaka kudhihirisha kwamba unampenda, ingawa pia wanandoa (waliohalalishwa) huitumia siku hii kuongeza mapenzi kwenye ndoa zao kwa kupeana zawadi na kutoana ‘out’, wakiwa katika mavazi maalum ya rangi nyekundu.
Ni matumaini yangu kwamba msomaji wangu utakuwa umepata mwanga kuhusu maana na tafsiri ya Valentines Day. Nakushauri na wewe usiwe miongoni mwa watu wanaofuata mkumbo kwa kuiadhimisha siku hii tofauti kabisa na maana yake halisi. Epuka kufanya ngono hovyo au kukesha gesti kwa kisingizio cha kuadhimisha Valentines Day kwani hiyo siyo tafsiri yake. 
#Happy Valentines Day.

No comments:

Post a Comment