Wachezaji wa Yanga katika moja ya mazoezi.
Picha|Maktaba na Khatimu Naheka.
YANGA na Azam zilikuwa zikiwania saini ya mchezaji wa Kimondo FC, Geofrey Mwasuya kwa ajili ya msimu ujao, lakini vijana hao wa Jangwani wamecheza akili sana na kuiacha Azam na utajiri wake kwenye mataa.
Azam ndiyo iliyokuwa ya kwanza kufanya mazungumzo na mchezaji huyo, lakini Yanga ilipostukia ikamtumia tiketi ya Ndege kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam.
Mchezaji aliposikia anapanda ndege kwa mara ya kwanza akapagawa na kuja Dar es Salaam haraka bila kujiuliza akamwaga wino Yanga huku Azam wakibaki wanashangaa.
Winga huyo amesaini mkataba wa miaka mitatu na habari zinasema kuwa Yanga walimsajili Mwasuya wakimtuma nahodha wao wa zamani Shadrack Nsajigwa ambaye pia ni kocha wa kikosi cha timu ya vijana ya timu hiyo alipewa kazi maalum ya kukamilisha usajili huo huku Azam wakimpa kazi hiyo meneja wao Jemedari Said.
Kiongozi huyo alisema kufanikiwa kwa Yanga katika usajili huo kulitokana na kutumia ujanja mdogo uliomchanganya winga huyo ambapo walimtumia tiketi ya ndege kutua jijini Dar es Salaam kukamilisha usajili huo jambo lililomchanganya mchezaji huyo.
“Hakuwahi kupanda ndege sasa alipoambiwa kwamba Yanga wamemtumia tiketi akachanganyikiwa kabisa, huku akatudanganya kwamba anauguliwa kumbe amekuja Dar es Salaam kusaini mkataba wa miaka mitatu hapo ndipo Azam walipopigwa bao,”alisema mmoja wa viongozi wa Kimondo.
Msemaji wa Kimondo Chris Kashilika alipoulizwa alikiri Mwasuya kusajiliwa na Yanga ingawa alisema klabu hiyo bado haijakamilisha taratibu zake.
“Taarifa hizo tunazo kwamba Mwasuya amesajiliwa Yanga ingawa mwenyewe alikuwa ametuficha lakini tunachoweza kusema ni kwamba bado Yanga hawana uhalali wa usajili huo kutokana na kuwa mchezaji huyo bado ana mkataba na Kimondo utakaomalizika mwakani na hawajakamilisha taratibu.”
Habari zinasema kwamba Yanga walikuwa hawana mpango sana na mchezaji huyo lakini baada ya kuona Azam wanamfuatilia kwa karibu na wao wakaamua kuingia kwenye kinyang’anyiro na kubaini kwamba mchezaji huyo ni mdogo na anaweza kuibeba Yanga miaka mingi.
#Mwananspoti.
No comments:
Post a Comment