*Waeleza wanavyoshawishiwa wakiwa shule.
Na Peter Ambilikile
WATOTO wa vigogo nchini wametajwa kuwa waathirika namba moja katika biashara ya dawa za kulevya. Wakati watoto hao wakiathirika kutokana na biashara hiyo, pia imeelezwa kuwa baadhi ya vigogo nchini ndio wanaongoza katika kusimamia biashara na wapo tayari kusimama kidete kutetea wanaojihusisha na dawa za kulevya. Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa miezi minne katika mikoa mbalimbali nchini, umebaini kuwa watoto wengi wa vigogo waliopo serikalini na kwenye taasisi za binafsi ndio walioathirika zaidi na matumizi ya dawa hizo aidha kwa kujua au kutojua.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, umeonesha wazi kuwa kuathirika kwa watoto wa vigogo hao, huenda ikawa laana ya Mungu kutokana na ukweli kuwa vigogo wengi ndio wenye kuhusika na biashara ya dawa za kulevya. Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya vijana ambao wameathirika na dawa za kulevya, ambapo kwa sasa wapo kwenye vituo vya kupunguza makali ya matumizi ya dawa za kulevya walisema, vijana wengi ambao wameathirika ni watoto wa vigogo nchini.
Walifafanua kuwa wamekuwa wakitumia dawa hizo, baada ya kurubuniwa na baadhi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya ambapo wamekuwa wakiwafuata watoto hao kuanzia shuleni. Akitoa ushuhuda, msichana anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 19, anayesoma Shule ya Sekondari Shaaban Robert jijini Dar es Salaam (jina tunalo), alisema muda wa kutoka shule unapofika kuna baadhi ya watu wenye asili ya kiarabu ambao huwafuata na kuwarubuni kwa kuwapa fedha na kuomba wakutane mbali ya eneo la shule.
Msichana huyo ambaye kwa sasa yupo kwenye kituo maalumu akipatiwa matibabu ya kuachana na matumizi ya dawa hizo kwenye Kituo cha Gongolamboto Sober House kilichopo Zanzibar (jina tunalo), amelazimika kukatisha masomo yake ya sekondari katika shule hiyo baada ya kuzidiwa na matumizi ya dawa hizo.
Aidha, alisema anajuta kukubali kushawishiwa na kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya, ambapo kwa sasa anapambana kujinasua ili kutoka kwenye matumizi hayo na kurejea hali yake ya zamani.
Aliongeza kuwa, baba yake ni mtumishi wa umma anayejiweza kifedha na amekuwa akitumia kila njia kuhakikisha anapata nafuu na ndio maana aliamua kumpeka katika kituo hicho.
"Wazazi wangu wapo tayari kutoa kila kitu kwa mtu atakayeniwezesha kurudi katika hali yangu ya zamani. Nilikuwa mtoto mzuri napenda shule, lakini hivi sasa nashindwa kwa sababu tu hizi dawa zimeingia akilini na kuniharibu kabisa.
"Natambua nafasi ambazo wazazi wangu wanazo serikalini na haya matumizi ya dawa za kulevya nilishawishiwa tu, kwa kuanza kuwekewa kwenye juisi na katika sigara. Waliokuwa wananishawishi waliniambia kuwa zinaongeza ufaulu shuleni," alisema mwanafunzi huyo.
Alisema Warabu hao walikuwa wakienda shuleni kwao wakiwa na magari ya kifari, na kwamba wakifika wanawarubuni kwa kuwataka kimapenzi na kisha wanaanza kuwafundisha kutumia dawa za kulevya.
Mbali ya yeye kuathirika na dawa hizo, alisema pia kuna marafiki zake wengi ambao nao ni watoto wa vigogo kuwa nao wameathirika na matumizi ya dawa hizo.
Mwanafunzi huyo ambaye ni mkazi wa Sinza Dar es Salaam, alisema baada ya wazazi wake kuhangaika na kutafuta ufumbuzi wa kumnusuru na matumizi ya dawa hizo ndipo walipoamua kumpeleka Zanzibar.
Akizungumzia baada ya kufika kwenye kituo hicho, alisema aliumia kwa kiasi kikubwa kwani hakupewa dawa za kulevya wakati alipokuwa anahitaji ili kuondoa maumivu mwilini. Msimamizi wa kituo hicho aliyejitambulisha kwa jina la Zulfa Issa, akizungumza hivi karibuni alisema binti huyo na wengine waliopo kituoni hapo wanaendelea vizuri. Mwanafunzi huyo wa Sekondari ya Shaaban Robert alisema huenda akarejea Dar es Salaam ili aendelee na masomo kwani hali yake inaendelea kuimarika siku hadi siku.
Uchunguzi uliofanywa Kituo cha Nyarungusu Sober House kilichopo Zanzibar, unaonesha kuna watoto wa vigogo waliopo kituoni hapo ambao wameathirika na matumizi ya dawa za kulevya. Watoto wengi ambao wameathirika wamekatisha masomo yao wakiwa kidato cha kwanza na wengine cha pili.
Msimamizi huyo alisema pia kuna baadhi ya wanafunzi wanaosoma vyuo mbalimbali nchini ambao wameathirika na matumizi ya dawa za kulevya.
Kutokana na uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, makala maalumu za uchunguzi zinatarajiwa kuanza kutolewa hivi karibuni, ambapo zitaelezea athari za dawa hizo na namna ya nguvu kazi ya taifa inavyopotea kutokana na biashara ya dawa za kulevya.
No comments:
Post a Comment