Binti, Anastazia Phillip (18) anayesumbuliwa na uvimbe ulioota mguuni.Chande Abdallah na Deogratius MongeLa
Mwanafunzi aliyemaliza kidato cha nne mwaka huu katika Shule ya Sekondari Kibasila, jijini Dar, Anastazia Phillip (18) mkazi wa Buza, amejikuta ameota uvimbe wa ajabu unaofananishwa na kibuyu.
MATESO MAKUBWA MIEZI 13
Kutokana na hali hiyo, msichana huyo amekuwa akiishi kwa mateso makubwa kwa miezi 13 mfululizo pasipo na matumaini ya kupona.
MAMA MZAZI ASIMULIA
Akisimulia kisa hicho, mama yake mzazi aliyejitambulisha kwa jina la Hellena Ringe alisema kuwa mara ya kwanza alimuona mwanaye akiugulia maumivu ya mguu mwishoni mwa mwaka jana akidai kuwa chanzo ni kujigonga wakati akiwa anahamisha dawati na wanafunzi wenzake.“Baada ya kujigonga ulianza uvimbe mdogo kama kipele huku akipata maumivu,” alisema mama huyo.
APELEKWA HOSPITALI YA AMANA
Akaongeza: “Baada ya kuwa analalamika kupata maumivu makali niliamua kumpeleka binti yangu Hospitali ya Amana ambapo alipigwa picha ya X-ray na kutakiwa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Muonekano wa uvimbe ulioota kwenye goti la mguu wa kulia wa Anastazia.
WAGUNDUA MFUPA KUSAGIKA
“Tulipofika Hospitali ya Muhimbili, kitengo cha mifupa cha Moi madaktari waligundua kuwa mfupa wa goti unaonekana kusagika na wakatushauri ukatwe ikiwa uvimbe utazidi kumkosesha raha.”
APELEKWA SHULE KUTAHINIWA KWA BAJAJ
Mama huyo alisema: “Kwa kuwa alikuwa hajamaliza kidato cha nne wakati uvimbe huu unajitokeza, nilikuwa nalazimika kumpeleka shule na kurudi nyumbani kila siku kwa Bajaj.“Huko shule nilikuwa nampandisha ghorofani kwenye madarasa. Nilifanya hivyo mpaka wakati wa mitihani yake ya kumaliza kidato cha nne mwaka huu, uzuri ni kwamba mwenyewe anapenda shule.”
BABA YAKE ALISHAFARIKI DUNIA
Akizungumzia msaada mama huyo anasema: “Kuna mtu aliniambia kwamba huko India wanatibu uvimbe huu, ningekuwa na uwezo ningempeleka mwanangu lakini mimi mwenyewe sina chochote na zaidi ni kwamba mimi ndiye baba na mama wa familia yangu kwani baba yake alifariki tangu mwaka 1994.”
Anastazia akilia kwa uchungu wakati akisimulia yaliyomsibu.
ASHINDWA KUONGEA, ALIA
Waandishi wetu walishindwa kuongea na msichana huyo kutokana na kila mara kulia.
MSAADA
Yeyote aliyeguswa na ugonjwa wa msichana huyu na anataka kumsaidia kwa hali na mali awasiliane kupitia namba 0713 165879 au 0752 264 127-Mhariri
Chanzo: GPL
No comments:
Post a Comment