Saturday, December 20, 2014

MAPENZI: ETI KUMBE SIMU ZA KISASA ZA KUTACHI NI SUMU MBAYA KWA MAPENZI??.. JIBU LIKO HAPA!

LEO nataka kuzungumza na nyinyi juu ya maendeleo ya teknolojia ya simu za ‘kutachi’. Simu hizi zimegeuka kuwa tatizo kubwa kutokana na wengi kuzitumia ndivyo sivyo.
Imefika wakati simu inamteka mtu akili kiasi cha kusababisha maafa makubwa katika suala la uhusiano. Wanandoa, wachumba wamekuwa wakiingia katika migogoro kila kukicha kutokana na mmoja wao kuwa bize pindi anapokuwa na mwenzake.
 Simu hizi zimewateka akili watu wengi kiasi kwamba kila wakati mtu anataka kubofya au kupangusa kama vijana wanavyosema.
Atataka kupangusa akiwa kazini, akiwa katika usafiri wa umma au wa binafsi na hata akifika nyumbani na kukutana na mpenzi wake ataendelea kufanya hivyo. 
Hata kama ametoka ‘out’ na mpenzi wake, bado mtu wa aina hiyo utamuona anaongea maneno machache na mwenzake huku muda mwingi akiuutumia kuperuzi mitandao mbalimbali tena mbaya zaidi mingi ni ya umbeaumbea tu! 
Ukiachana na suala la kuperuzi mitandao, tathmini isiyo rasmi inaonesha miongoni mwa vitu vinavyowapotezea muda mwingi watu katika simu hizo ni matumizi ya magrupu ya mitandao mbalimbali ambayo wanayaanzisha kwa kundi la watu fulani.

Eti utasikia hili grupu la wafanyakazi wenzangu, hili ni la wanandugu na lingine ni la kufundisha mambo fulanifulani wanayoyajua wenyewe. Hayana maana yoyote!Wataanzisha kundi ambalo linamlazimu kujibu au kuchangia mjadala fulani ambao pengine umeanzishwa na kumhusisha yeye hivyo hawezi kukubali kukaa kimya pindi wenzake wanapochangia.

Asilimia kubwa ya mijadala ambayo inaonekana kupendwa zaidi na watu inaonekana si yenye tija, wanapenda vitu vya umbeaumbea kujua fulani anatoka na nani au fulani kammwaga fulani.
Vitu hivyo vinawafanya wanawehuka kabisa, maana mtu hujikuta hata akikosea maneno pindi anapoongea na mpenzi wake na kutaja neno ambalo alikuwa akiliandika katika grupu alilokuwa akichangia kupitia simu yake hiyo ya kisasa. 
Kwa jinsi alivyonogewa na umbea, anasahau kabisa kwamba mumewe anapaswa kupelekewa maji bafuni au kuandaliwa chakula, achilia mbali vile vikorombwezo vya kimahaba ambavyo wapendanao wanapaswa kupeana pindi wanapokuwa pamoja hususan nyumbani au chumbani.
Ili asipitwe na mjadala kwenye grupu fulani, yuko radhi amuite hausigeli na kumtuma amfanyie kila kitu ambacho kilipaswa kufanywa na yeye.Achilia mbali masuala ya mapenzi, kuna wakati mwenzake atataka kukaa na kujadili mambo ya kifamilia, suala hilo pia linaweza kushindikana eti tu kwa sababu mwenzake yuko bize na simu. 
Tatizo hapa linakuwa ni aina ya mtu ambaye utakuwa naye. Kuna mtu anaweza kukutolea uvivu na kukwambia kwamba unamkwaza kutokana na kitendo chako cha kutomjali lakini kuna mwingine hawezi, atakaa nalo moyoni na kufanya maamuzi yake anayoyajua mwenyewe.

No comments:

Post a Comment