Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Rajabu Rutengwe kuomboleza vifo vya watu 11 ambapo wengine kadhaa walijeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea tarehe 27 Novemba, 2014.
Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Mkanyageni Mkoani Tanga baada ya basi dogo aina ya Toyota Coaster Na. T 410 BJD iliyokuwa ikitoka Tanga Mjini kuelekea Lushoto kugongana na Lori aina ya Scania Na. T 605 ABJO.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kupotea ghafla kwa maisha ya watu 11 na wengine kadhaa kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea katika Mkoa wako wa Tanga”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake na kuongeza:
“Naomba upokee salamu zangu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kutokana na vifo hivyo, na kupitia kwako, naomba salamu za pole ziwafikie watu wote waliopotelewa na ndugu na jamaa zao kwenye ajali hiyo”.
Rais Kikwete amesema anawaomba wote waliopoteza ndugu na jamaa zao kwenye ajali hiyo wawe watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, na amewahakikishia kuwa yuko pamoja nao katika kipindi chote cha maombolezo.
“Kwa wote waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo, namwomba Mungu awajalie ahueni na wapone haraka, ili warejee tena katika hali zao za kawaida. Namwomba Mola azipokee na kuzilaza mahala pema peponi Roho za Marehemu wote, Amina”, amemalizia kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
27 Novemba, 2014
No comments:
Post a Comment