Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Meza Kuu-Katikati),
akizungumza na wawakilishi wa Kampuni mbalimbali zinazohusika kusambaza
umeme vijijini kutoka India, China na Sri Lanka zinazofanya kazi katika
Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuhusu utekelezaji wa miradi husika.
Wawakilishi
wa Kampuni mbalimbali zinazohusika kusambaza umeme vijijini kutoka
India, China na Sri Lanka zinazofanya kazi katika Mikoa ya Nyanda za Juu
Kusini Magharibi pamoja na baadhi ya Mameneja wa Tanesco wa Mikoa
husika, wakitoa mrejesho kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo (Meza Kuu – Katikati), kuhusu hatua iliyofikiwa katika
utekelezaji wa Miradi husika. Kulia kwa Waziri Muhongo ni Naibu Waziri
wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Charles Kitwanga na
kushoto kwa Waziri ni Kamishna Msaidizi wa Nishati sehemu ya Umeme,
Mhandisi Innocent Luoga.
Mkurugenzi
Mkuu wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Dk. Lutengano Mwakahesya
akizungumza katika mkutano baina ya Waziri wa Nishati na Madini na
kampuni zinazosambaza umeme vijijini kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Mwakahesya aliahidi kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha
miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa.
*******
Na Veronica Simba
WAZIRI
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amezitaka Kampuni
zilizopewa tenda kusambaza umeme vijijini kukamilisha kazi hiyo kwa
wakati na kwa kiwango kinachotakiwa vinginevyo watanyang’anywa tenda
hizo.
Aliyasema
hayo mwishoni mwa wiki mjini Dodoma katika Mkutano baina yake na
wawakilishi wa Kampuni husika kutoka India, China na Sri Lanka
zinazofanya kazi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi pamoja
na Mameneja wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) wa mikoa hiyo na Wakala
wa Umeme Vijijini (REA).
Profesa
Muhongo aliitisha Mkutano huo kwa lengo la kupokea taarifa kutoka kwa
Watendaji wa Kampuni hizo kuhusu hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa
miradi ya umeme vijijini kabla ya kutembelea miradi hiyo kwa mara
nyingine kama ambavyo amekuwa akifanya mara kwa mara kujiridhisha na
maendeleo yake.
Akizungumza
katika Mkutano huo mara baada ya kupokea taarifa za utekelezaji kutoka
pande zote, Waziri Muhongo alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa REA, Dk.
Lutengano Mwakahesya kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo unafuatiliwa
kwa ukaribu na kusitisha tenda mara moja kwa kampuni zitakazobainika
kutotimiza makubaliano ya mkataba walioingia.
“Fuateni
utaratibu wa kisheria kwa kutumia vifungu vilivyomo kwenye mkataba
vinavyoelekeza kuchukua hatua stahiki kwa kampuni isiyotekeleza wajibu
wake ipasavyo,” alisisitiza Muhongo.
Aliongeza
kuwa Serikali imedhamiria kuhakikisha inatimiza ahadi yake ya kuwapatia
Watanzania umeme ili wajikwamue katika lindi la umaskini kwa kukuza
kipato chao na cha Taifa kwa ujumla hali itakayofanya Tanzania kufikia
uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
“Yeyote
atakayetukwamisha au kuturudisha nyuma katika kufikia malengo yetu ya
kuwaondolea Watanzania umaskini, tutapambana naye na kamwe hatutampa
nafasi,” alisema Muhongo.
Vilevile,
aliwataka Mameneja na watendaji wengine wa Tanesco kuachana na
utamaduni wa kukaa ofisini na kusubiri ripoti za utekelezaji wa miradi
badala yake watembelee miradi wanayosimamia na kuhakikisha kazi
inafanyika kama inavyotakiwa.
Aidha,
Waziri Muhongo aliwataka wakandarasi waliopewa tenda husika kuwa
wakweli na waaminifu na kuachana na tamaa hususan wanapopewa kazi ambayo
wanajua hawana uwezo wa kuitekeleza ipasavyo ili kuwapa nafasi wengine
wenye uwezo huo.
Alisema
ni bora kwa Mkandarasi kukubali kazi anayoimudu ili aifanye kwa ubora
unaotakiwa na hivyo kujiongezea sifa za kupewa kazi nyingine kuliko
kuomba kazi kubwa asiyoweza kuitekeleza kikamilifu na matokeo yake
anaharibu na kupoteza sifa ya kufikiriwa kupewa kazi nyingine.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati,
Charles Kitwanga aliwataka wote wanaohusika na utekelezaji na usimamizi
wa miradi hiyo ya kusambaza umeme vijijini kutimiza wajibu wao kwa
vitendo.
“Achaneni
na maneno maneno, mimi nataka kuona vitendo, nataka kuona matokeo,”
alisisitiza na kuongeza kwamba hakuna sababu ya Wakandarasi kusuasua
katika utekelezaji wa miradi hiyo kwani walioomba wenyewe wakijinadi
kuwa wanaweza.
Naye
Kamishna Msaidizi wa Nishati Sehemu ya Umeme, Mhandisi Innocent Luoga
aliwataka Wakandarasi hao kujituma na kufanya kazi inavyostahili pasipo
kusubiri kufuatwa-fuatwa na kuhimizwa kwa suala ambalo ni wajibu wao.
Wakichangia
mawazo katika Mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Edmund Mkwawa na
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala huo, Dk. Mwakahesya waliahidi kufanya kazi
bega kwa bega na wadau mbalimbali wa sekta hiyo ili kuhakikisha
Watanzania hususan walioko vijijini wanapatiwa nishati ya umeme kama
Serikali ilivyodhamiria na kuahidi.
No comments:
Post a Comment