Thursday, September 4, 2014

DIASPORA NA URAIA PACHA (DUAL CITIZENSHIP)

Kagutta N.Maulidi, Mwenyekiti, Tanzanian Diaspora Committee in Italy.
*************
TUNAENDELEA kufuatilia majadiliano ya wajumbe maaluum wa bunge la katiba si vibaya tukaweka msisitizo au kuwakumbusha wajumbe wetu kuhusu mada iliyopo katika rasimu ya katiba sura ya tano inayozungumzia urai pacha. Nchi yetu bado haitambui uraia wa nchi mbili, kwa maana kuwa ukichukua uraia wa nchi nyingine unapoteza haki ya Urai wako wa Tanzania.

Tunashukuru kuwa swala hili limeingizwa katika rasimu ya pili ya katiba,ili liweze kujadiliwa .Sisi Watanzania tunaoishi nje ya nchi ni matumaini yetu kuwa wajumbe wa bunge maalumu wataliangalia swala hili kwa mapana zaidi na kulikubali kwa faida ya watanzania na nchi yetu kwa jumla.

Wengi wa watanzania wanaoishi nje(Diaspora) wamelazimika kuomba uraia wa nchi wanazoishi ili kupata haki zao baada ya kuishi na kufanya kazi kati katika nchi hizo kwa muda mrefu.

Watoto:
Zipo nchi zinazowatambua moja kwa moja wanapozaliwa kuwa ni raia lakini pia bado zipo nchi hawatoi uraia kwa watoto wanapozaliwa mpaka wanapofikisha miaka 18.

Kwa wale ambao wanapewa urai kwa kuzaliwa, moja kwa moja wanakuwa hawawezi tena kuchukua urai wa wazazi wao, na kuendelea kuwa wageni katika nchi ya asili yao Tanzania. 

Watoto ni hazina kubwa ya taifa letu ,kwa kuwapa uraia wa nchi ya asili yao inawapa fursa ya kuliwakilisha taifa letu katika michezo ya kimataifa na kuliletea sifa na maendelleo taifa letu. Watapata fursa ya kuutumia ujuzi wao katika kuchangia maendeleo ya taifa letu kiuchumi.

Watoto wa watanzania pamoja na kuwa wamezaliwa ughaibuni lakini wana mapenzi makubwa kwani wanajua wazi Tanzania ndio kwao kiasili.

Faida za Uraia pacha:
Kwa maoni ya wengi na hivyo ndivyo ilivyo ,sheria ya urai pacha itawapa msukumo diaspora katika kushiriki zaidi katika kuchangia maendeleo ya taifa letu,kiuchumi,kisiasa na kijamii.

Watanzania watakuwa wamepata fursa nzuri ya kuwekeza nyumbani na kuongeza ushawishi kwa wawekezaji wa nje kutoka sehemu wanazoishi kuwekeza Tanzania.
Ni imani yangu kuwa asilimia 100% ya watanzania hawakuondoka nchini kwa kuto ipenda nchi yao bali wametoka katika kutafuta,kusaidia familia zao na wazazi wao nyumbani,bado wana mapenzi makubwa na nchi yao,kutokuwepo sheria ya urai pacha ni kuwabana watanzania hao na kuwasababishia kukosa haki na huduma muhimu katika sehemu wanazoishi.

Mkiangalia katika mitandao utaona jinsi watanzania hawa walivyo na mapenzi na nchi yao,wanajionyesha wazi kabisa hasa wanapo sherehekea sikukuu za kitaifa kwa pamoja na kujaribu kuwa karibu na nchi yao katika siku zenye kumbukumbu kubwa kwa taifa letu.
Wanapo pata likizo inawagharimu kulipia visa ambayo pia ina muda wa kukaa nchi ambayo ndiko kuna kila kitu chake ,wazazi,ndugu,marafiki nk. 

Serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete imetoa kipaumbele na kutambua mchango wa diaspora kwa taifa. serikali imeona umuhimu wa kuwashirikisha diaspora katika ujenzi wa nchi yao na kuwapa nafasi za kuchangia maendeleo kiuchumi,kisiasa na kijamii,hivyo ili kuongeza kuwapa nafasi diaspora kutoa ushirikiano zaidi katika maendeleo ya nchi yetu,Sheria ya uraia pacha ipite,tunaomba ndugu wajumbe mkumbuke kwamba wapo watanzania wengi nje ya nchi wenye ujuzi mbalimbali ambao wangeweza kulitumikia taifa lao kama raia na kupunguza gharama za kuajiri wageni ambao wengine wana ujuzi hata chini ya watanzania hawa. 

Wakati umefika wa kufanya hivyo,bila kuangalia tu kuwa eti diaspora wanataka huku na kule. Tuchukue mifano ya mataifa mengine ambayo sheria hii ipo siku nyingi katika nchi zao,hakuna hasara wala madhara kabisa ya kupisha sheria ya urai pacha, zaidi ni faida kwa raia na nchi kwa jumla. 

Mpaka sasa kuna jumuiya nyingi za watanzania zilizoundwa nje ya nchi,lengo na madhumuni ni kuwakusanya watanzania kuwa pamoja na kushirikiana kwa kila hali,kushauriana na kuweza kushiriki katika maendeleo ya nchi yao.Watanzania hawa pamoja na michango yao mikubwa kwa familia zao (remittance), lakini wana lengo la kupanga mikakati ya pamoja na kubuni mbinu za kushiriki katika maendeleo ya taifa.

Kongamano za diaspora ni ishara ya wazi inayoonyesha jinsi gani wazalendo hawa walivyo na nia ya maendeleo na mapenzi ya nchi yao. Wajumbe wa Bunge maalumu la katiba pamoja na kujadili vipengele vyote muhimu vya rasimu ya katiba ambavyo ndio msingi na muuongozo wataifa letu,tunawaomba mlijadili kwa kina suala hili kwani tunaolipigania tuko nje lakini sio sababu ya kutotiliwa makazo.

Ni matumai yetu suala hili mtalipitisha katika katiba mpya ya nchi yetu kwa faida yetu,nchi yetu na vizazi vijavyo. Kwa kufanya hivyo tunaamini kuwa haki ya kidemokrasia ambayo tumekuwa tukinyimwa watanzania ughaibuni itapatikana.Uwekwe utaratibu mzuri ili na sisi tuweze kushiriki katika kuchagua viongozi wetu hasa uchaguzi mkuu wa rais kuanzia 2015.

MUNGU IBARIKI AFRIKA
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU LIBARIKI BUNGE MAALUMU LA KATIBA

Kagutta N.Maulidi
Mwenyekiti
Tanzanian Diaspora Committee in Italy.
e-mail: tanzaniaitalia.sc.coop@gmail.com 
Tel/fax +39 081 0200142 cell. +39 398 85 83370

No comments:

Post a Comment