Friday, September 5, 2014

ATHARI ZA UVUVI WA MABOMU TANZANIA

Tanzania inasifika sana kwa mazingira yake ya bahari.
''Uvuvi wa mabomu unaharibu mazingira ya chini ya bahari ambayo huwezesha samaki kuzaana na hiyo imetuathiri sana sisi tunaovua kwa kutumia nyavu kuvua -idadi ya samaki imepungua sana,sio kama hapo awali''.
Anasema mvuvi mmoja ambaye aliomba jina lake kubanwa,huku akijiandaa kuingia baharini kuvua pamoja na wenzake.
''Tunawaripoti kwa polisi wale wanaotumia mabomu lakini wanapokamatwa wanatoa hongo na kuachiliwa na wanapogundua tumewaripoti wanaweza kuandana chombo chetu na kuturushia vilipuzi, wanatishia kufanya hivyo na ndio sababu wakati mwingine tunaogopa kusema''anasema
Kwa miaka minane mvuvi huyo amekuwa akitegemea maji ya Bahari Hindi ambayo yana utajiri wa maelfu ya samaki aina mbalimbali. Bahari hindi hukumbatia Tanzania kwa umbali wa maelfu ya kilomita. Kila siku boti za uvuvi huelea juu ya bahari hiyo. Lakini sasa uvuvi wa kutumia vilipuzi unatishia kuangamiza raslimali hiyo muhimu. Baadhi ya wavuvi hutumia vilipuzi hivyo ili kuweza kuvua samaki wengi.
Kulingana na shirika la Smart Fish, ambalo linashirikiana na serikali kukabiliana na tatizo hilo, Tanzania ndiyo nchi pekee barani Afrika ambapo uvuvi huo haramu unafanyika kwa kiwango kikubwa. Uvuvi huo hufanyika katika maeneo mengi ya pwani kuanzia Dar es Slaam,Mtwara hadi Tanga, visiwani, na kumekuwepo ripoti za mabomu kutumiwa katika bahari ya Kaskazini mwa Zanzibar.
'Maji yanayolipuka'
Wavuvi ambao hutumia nyavu kuvua wanalalamika kuwa Samaki wamekuwa wachache.
Kulingana na Baraka Mngulwi, ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa uhifadhi wa raslimali za uvuvi nchini Tanzania, vilipuzi hivyo hupatikana kwa njia haramu kutoka maeneo ya uchimbaji madini, utengezaji barabara na wakati mwingine watu huvitengeneza nyumbani.
Kulingana na Mngulwi, watu wamekuwa wajanja kiasi cha kuyatengeneza mabomu hayo nyumbani kwa kutumia kemikali fulani ambazo zina uwezo wa kulipuka.
Vilipuzi hivyo huwashwa moto na kurushwa ndani ya bahari. Mlipuko ambao hutokea huwashtua na kuwaua samaki na hapo wavuvi hutumia nyavu kuwavua.
Baadhi wanasema wanapowaripoti wanaotumia mabomu kuvua huandamwa.
Wataalam wanasema mlipuko mmoja unatosha kuua samaki na viumbe vyote hai vilivyo umbali wa mraba mita 20-na kuua Samaki wapatao 400 kwa wakati mmoja. Matokeo yake ni uharibifu mkubwa wa mazingira ya chini ya bahari ambayo huwezesha Samaki kuzaana.

No comments:

Post a Comment