Wednesday, July 2, 2014

WATOTO WAISHIO KWENYE MAZINGIRA MAGUMU, WANAOISHI NA VVU WAZIDI KUNYANYAPALIWA

Mahmoud Ahmad,Arusha.
WATOTO waishio kwenye mazingira magumu na yatima hususani wanaoishi na virusi vya ukimwi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kunyanyapaliwa na wazazi na hata walimu mashuleni hali ambayo imekuwa ikiwawia vigumu watoto hao kuendelea na masomo.
Aidha unyanyapaa kwa watoto yatima wanaoishi na virusi vya ukimwi imekuwa ni changamoto kubwa kwao ambapo asilimia kubwa ya watoto wamekuwa wakikosa haki zao za msingi hususani elimu kutokana na hali hiyo.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa shirika la Sorode Organization la jijini hapa, Sophia Justine wakati akizungumza na watoto na walezi waliohudhuria katika harambee ya kuchangia bweni kwa ajili ya watoto yatima wa kike wanaolelewa katika kituo cha Faraja ambapo shs 1 milioni zilipatikana huku zikihitajika shs 50 milioni.
Alisema kuwa, kumekuwepo na unyanyapaa wa hali ya juu unaofanywa na walimu katika shule mbalimbali baada ya kupewa taarifa kuhusu watoto hao hali ambayo imekuwa ikisababisha watoto hao kutengwa na wengine na hata wakati mwingine kuchukiwa kabisa na walimu na wazazi kwa ujumla.
Sophia alisema kuwa, watoto hao wanahitaji kupatiwa haki zote za msingi kama wanavyopata watoto wengine badala ya kunyanyapaliwa na kutengwa na jamii kama watoto wasiofaa na kustahili kama wengine kitendo ambacho kimekuwa kikiwapa wakati mgumu kuishi katika jamii.
‘sisi shirika letu hili tumekuwa tukitoa elimu kwa jamii mbalimbali ikiwemo vituo mbalimbali vya watoto yatima ili kuweza kujua haki za mtoto ,na changamoto zinazowakabili ndio maana leo tukaamua kuandaa harambee hii ambayo ndo mwanzo tu lengo ni kuhakikisha fedha za bweni zimepatikana kwa ajili ya kusaidia watoto hawa wa kike’alisema Sophia.
Naye Mkurugenzi wa kituo hicho cha kulelea watoto yatima cha Faraja ,Faraja Maliaki alisema kuwa, kituo hicho kina jumla ya watoto 200 ambapo kati ya hao watoto 30 wanaishi na virusi vya ukimwi na watoto 48 wakiwa hawajulikani kabisa walipotokea wala makabila yao kutokana na kuokotwa baada ya kutupwa baada ya kuzaliwa.
Alisema kuwa, kituo hicho kimekuwa kikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa bweni la wasichana ambapo kituo kina idadi ya wasichana 103 ambao wamekuwa na uhitaji huo wa bweni.
Faraja aliongeza kuwa, watoto hao wamekuwa wakilala chini na wengine kusongamana kwenye kitanda kimoja kutokana na kutokuwa na bweni ,hivyo aliomba wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia bweni la watoto hao ambao wanaendelea kukua siku hadi siku.
Aidha alielezea changamoto nyingine kuwa ni pamoja na malazi, chakula,mavazi,kwani wakati mwingine wamekuwa wakila mlo mmoja tu kwa siku huku idadi yao ikiendelea kuongezeka kila siku.

No comments:

Post a Comment