WATAFITI katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba cha Temple, Marekani wamegundua dawa ya kuangamiza Virusi Vya Ukimwi (VVU) ambayo ni ya uhakika zaidi ukilinganisha na zilizowahi kupatikana katika tafiti za awali duniani.
Dawa yao inaweza kutumika kwa tiba ya wanaoishi na VVU na kinga kwa wale ambao bado hawajaambukizwa.
Mmoja wa watafiti hao, Dk Kamel Khalili aliwaambia waandishi wa habari juzi mjini Philadelphia, Marekani kuwa tofauti na utafiti mwingine, wao wamegundua namna ya kukiondoa kirusi kilichoingia kwenye kinasaba (DNA) ndani ya CD4 na kukitoa nje na hatimaye kukiua.
Alisema dawa hiyo inafanya kazi hiyo bila kuathiri seli za mwili wa binadamu.
Dk Khalili alisema ugunduzi wao ni wa hali ya juu zaidi kwa sababu teknolojia ya kutengeneza dawa hiyo ni tofauti na nyingine zilizokwisha kugunduliwa ambazo hazina uwezo wa kupenya ndani ya seli za binadamu, bali kuathiri tu VVU vilivyopo nje yake, ndani ya mfumo wa damu.
“Dawa yetu inakivuta kirusi nje ya seli (CD4) bila kuiathiri seli yenyewe na kukiua. Hivyo dawa hii itatumika kwa muda fulani na kuua virusi vyote mwilini na hakuna haja ya kuitumia wakati wote kama ilivyo dawa ya kufubaza VVU (ARV).”
ARV huangamiza VVU vilivyopo kwenye damu na kuendelea kuviacha hai vile ambavyo tayari vimeingia ndani ya CD4, hivyo kufanya virusi kuzuka upya pindi mwathirika anapoacha kutumia dawa.
Mmoja wa wataalamu katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Kituo cha Mbeya (NIMR-MMRC), Clifford Majani ameuelezea utafiti huo kama mwanga mpya katika teknolojia ya kukabili VVU.
“Kama imepatikana teknolojia ya kukiondoa kirusi ndani ya seli ni hatua nzuri ya kukabili VVU. Hili lilionekana kuwa gumu mwanzoni,” alisema Majani.
Alisema imekuwa vigumu kuua kirusi kikiwa ndani ya seli na hata baadhi ya wanasayansi wamejaribu kutengeneza dawa itakayotambua seli zilizoathirika ili ziuawe lakini hilo likawa gumu.
“Inaweza ikapatikana dawa ya namna hiyo (inayoua seli zilizoathirika) lakini ikawa inaathiri vitu vingine ndani ya mwili. Hilo halikubaliki. Kikubwa katika ugunduzi huo ni dawa kuweza kukifuata kirusi kinakojificha na kukiondoa, jambo ambalo dawa nyingi zimeshindwa zikiwamo ARV,” alisema.
Hata hivyo, Majani alisema changamoto ambayo inaweza kujitokeza katika majaribio ya dawa hiyo ni usalama wakati wa matumizi.
“Lazima dawa hiyo ichunguzwe isije ikawa inaathiri viungo vingine pamoja na utendaji wa mwili kwa ujumla. Maana hapo ndipo dawa nyingi zinaposhindwa… Tusubiri tuone hii inaweza kuwa na matumaini zaidi,” alisema Majani.
MKUTANO WA UKIMWI
Ugunduzi huo umekuja wakati wanasayansi, waunda sera na wadau wa mapambano ya VVU wakiwa wanatoa kauli za kukata tamaa kwenye mkutano wa Ukimwi unaomalizika kesho huko Melbourne, Australia.
Wanasayansi kadhaa wanaotoka kwenye taasisi kubwa za utafiti za VVU wameweka wazi kuwa tafiti nyingi zilizokuwa na matumaini zimeshindwa kufanya kazi kwa asilimia 100 baada ya dawa zake kufanyiwa majaribio kwa sababu dawa zake zinapotumika, vipimo huonyesha wamepona lakini baada ya muda VVU hurejea upya.
“Kinachoonekana ni kwamba virusi hivi hujificha sehemu fulani ya mwili ili visiathirike na kusubiri mtu aache dawa ili virejee upya kushambulia CD4,” alisema Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti ya wa Magonjwa ya Kuambukiza na Kinga ya Peter Doherty ya Australia, Profesa Sharon Lewin.
DAWA MPYA INAVYOFANYA KAZI
Dk Khalili alisema wametengeneza dawa yao kwa protini maalumu ambayo inakata sehemu ya seli iliyoshambuliwa na kirusi cha Ukimwi na kukivuta nje.
Baada ya kukivuta, dawa huachana na seli hiyo na kuiacha ikijitibu yenyewe na kupona kabisa kiasi cha kuendelea na kazi zake za kinga mwilini mwa binadamu bila tatizo.
VVU kwa kawaida hushambulia seli kinga aina ya CD4 na kuzifanya kama kiwanda cha kuzalishia virusi vingine.
Kwa kawaida seli ikishaingiliwa na kirusi, huacha kazi yake ya kinga ya mwili na badala yake kuchukua jukumu la kutengeneza VVU.
“Dawa yetu inafanya kazi kwa haraka, kwa makini na bila kuathiri seli,” alijigamba Dk Khalili.
Alisema tayari imefanyiwa majaribio maabara na kuonekana inafanya kazi vizuri na sasa wamehamishia majaribio kwa wanyama.
Katika maabara, alisema dawa hiyo ilifanyiwa majaribio kwa damu ya binadamu na ikaonyesha kufanya kazi kwa asilimia 100.
Dk Khalili anaamini kwamba majaribio hayo yatawachukua miaka michache... “Lakini tunaamini ni mfumo ambao utaweza kufanya kazi vizuri kwa binadamu.”
Alisema wanachofanya sasa ni kuangalia mfumo ambao utakuwa mzuri zaidi kwa ajili ya tiba ya binadamu.
Kwa namna teknolojia ya dawa hiyo ilivyo, alisema wanaweza kuitumia kwa ajili ya kuwatibu wale ambao tayari wameambukizwa na hata kuwakinga wale ambao siyo waathirika.
Uzuri wa dawa hiyo, pia alisema inaweza kutumiwa na mtu ambaye anatumia ARV pasipo kuingiliana kiutendaji.
Ugunduzi wao ulichapishwa kwenye Jarida la Taifa la Elimu ya Sayansi la National Academy of Science la Marekani na kuonekana kuvuta hisia za wengi.
HALI YA UKIMWI DUNIANI
Akizungumza kwenye mkutano wa Melbourne, Profesa Lewin alisema tafiti za sasa zinaonyesha kuwa karibu watu milioni 14 duniani wanaishi na VVU.
Alisema mamilioni ya watu hao wamekuwa wakisaidiwa kwa kutumia ARV, wakati huu ambao bado hakuna kinga wala tiba, inayoaminika.
Alisema ingawa tafiti nyingi hazijaonyesha matumaini waliotarajia ya kupata kinga na chanjo, bado juhudi zinaendelea ili kuhakikisha wanafikia mahali HIV inakuwa haina nafasi katika mwili wa mwanadamu.
Alisema pamoja na matokeo hasi ambayo yamejitokeza kwenye tafiti nyingi, bado anaamini kwamba ipo siku chanjo na tiba vitapatikana.
Wanasayansi waliohudhuria mkutano huo waliitaka dunia isiogope kutokana na kushindwa kwa baadhi ya tafiti kama ilivyokuwa kwa mtoto wa Jimbo la Mississippi, nchini Marekani ambaye alitangazwa amepona na baadaye virusi vikaibuka upya.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment