Wednesday, July 9, 2014

MAUAJI YA MAMA WA GEITA YAMPASUA KICHWA MKUU WA WILAYA YA GEITA *PICHA*

Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Geita Omary  Mangochie akiweka udongo kwenye kaburi la Lydia Kaiche aliyeuawa kwa kukatwa mapanga.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Omari  Mangochie akiwahutubia wananchi wa Mtaa wa Misheni jana kwenye msiba wa kumuaga Lyidia Kaiche aliyeuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiofahamika akiwa nyumbani kwake.
Mkuu wa Wilaya akiweka shada kwenye Kaburi la Lydia Kaiche aliyeuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiofahamika na kutokomea kusikojulikana.
Picha zote naValence Robert-Malunde1 blog- Geita. 

VIJANA wote wanaoishinda  vijiweni wakicheza pool wametakiwa kuacha tabia hiyo mara moja  kwani msako wa kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kwa uzururaji unaanza hivi karibuni kutokana na matukio ya mauaji ambayo yamekuwa yakitokea kila kukicha na kuuchafua mkoa wa Geita.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Geita Omary Mangochie kwenye msiba wa kumzika mama mmoja aliyejulikana kwa jina la Lyidia Kaiche  (55) wa mtaa wa misheni wilayani Geita aliyeuawa kwa kucharangwa mapanga juzi na watu wasiofahamika wakati akisikiliza taarifa ya habari .
Mangochie alisema mauaji ya vikongwe yanayoendelea katika mkoa wa Geita yanasikitisha na huenda yanafanywa na vijana wasiokuwa na kazi wanaoshinda vijiwe vya kahawa  na kuangalia luninga  huku wakicheza pool.

Mkuu huyo wa wilaya alitangaza kuanza msako wa kufunga pool zote na baa zisizofaa zinazotumika kwa kuwaficha vijana waovu.
Mangochie aliongeza kuwa mauji ya vikongwe yanauchafua mkoa wa Geita na yeye kama mkuu wa wilaya hawezi kuona watu wanazidi kufa tena wanaouawa ni akina mama tu hivyo kuwataka wenyeviti wa mitaa na watendaji wa kata zote kuorodhesha vijana wote wanaoishi nao kwenye mitaa na kata zao kabla msako mkubwa haujaanza kwani msako huo utakwenda Nyumba hadi Nyumba bila kujali nani wala nani.
"Jamani Wananchi mliohudhuria kwenye msiba huu tusaidiane kuwapata wauaji kwani tunaishi nao kwenye majumba yetu na kwenye familia zetu tunawajua, mimi kama Mkuu wa Wilaya nileteeni taarifa za watu hao watakamatwa na mkiona watu wanaingia kwenye mitaa yenu hamuwajui toeni taarifa",Alisema Mangochie
Naye Mwinjilisti wa kanisa la A.I.C.  Kalangalala Marco Madoshi katika mahubiri yake ya kumuombea marehemu alisema kuwa watu wanaowaua wenzao kwa imani za kishirikina wanatenda dhambi kubwa sana kwani hata Mungu hapendi kuona mauaji kama hayo yanaendelea katika mkoa wa Geita.
Aidha aliitaka familia hiyo iliyoondokewa na mpendwa wao kumwamini Mungu kuliko kwenda kwa waganga na kumtafuta mchawi nani na kuongeza uhasama kwa ndugu na jamaa.
‘’Jamani hata hawa vijana wasiokuwa na kazi wanashinda kwenye vijiwe wanacheza pool na huku jioni wanakunywa bia wanapata wapi pesa kama sio wanakodiwa na kwenda kuwauwa vikongwe hasa kina mama, mimi naungana na mkuu wa Wilaya wakamatwe vijana wote nami nitasaidia msako huo’’ alisema Mwinjilist huyo.
Na Valence Robert
Malunde1 blog, Geita

No comments:

Post a Comment