Friday, July 25, 2014

MATUMAINI RELI YA KATI SASA YAANZA KUONEKANA


MATUMAINI ya kuboreshwa kwa Reli ya Kati kwa lengo la  kuimarisha usafirishaji wa abiria na mizigo, yanazidi kuonekana baada ya serikali kuingiza mabehewa 25, ambayo ni maalumu kwa usafirishaji wa vifaa vya ukarabati wa njia hiyo.
Mabehewa yaliyopokewa jana jijini Dar es Salaam ni ya kubebea kokoto, ambayo yametoka India huku yakielezewa kuwa ni miongoni mwa vitendea kazi muhimu katika mkakati mzima wa kuboresha reli hiyo ya kati.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe aliyepokea mabehewa hayo, alisema mwanzoni mwa mwaka ujao, Reli ya Kati itakuwa imeimarika kwa ajili ya kuwezesha, siyo tu usafiri wa abiria, bali pia mizigo.
Alisema mabehewa hayo yenye thamani ya Sh bilioni 4.316, yatatumika kwa kubeba na kusafirishia kokoto kutoka sehemu zinakozalishwa na kupeleka kwenye maeneo kwa ajili ya kushindilia reli wakati wa matengenezo ya njia hiyo.
“ Hii itasaidia kuimarisha njia ya reli na kuwezesha kupitisha mizigo na abiria kwa usalama zaidi. Ni matarajio yangu TRL watayatumia vizuri ili yaweze kutumika kwa muda ujao,” alisema.
Akizungumzia huduma duni inayotolewa na  Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Mwakyembe alisema: 
“Ni lazima TRL ishindwe kutoa huduma nzuri kwa sababu haina vifaa na huwezi kuwalaumu. Kwa hali iliyopo kulikuwa na njia mbili; kusimamisha kabisa huduma au kuimarisha.”
“Mwaka 2002, TRL ilikuwa na vichwa zaidi ya 50 na mabehewa 2,200, leo tunaongelea vichwa vya treni vinane na mabehewa chini ya hapo, sasa vichwa vinane kutumika kwa treni ya mizigo na abiria hakutaweza kuwa na ufanisi,” alisema.
Waziri Mwakyembe alisema serikali imejipanga kuhakikisha Reli ya Kati, inaimarika kwa kuagiza vifaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vichwa vya treni na mabehewa ya mizigo na abiria.
Alisema kati ya Agosti na Desemba,  itapokea mabehewa ya mizigo 274, mabehewa ya breki 34 na mabehewa 22 ya abiria.
Mwakyembe alisema kati ya Januari na Mei mwakani, serikali itapokea vichwa vya treni vipya 13, chini ya mradi unaotekelezwa na Kampuni ya EMD ya Marekani.
“Hatua hii ni sehemu ya Mpango wa Matokeo Mkubwa Sasa (BRN), Wizara ya Fedha imefanya kazi kubwa kwani wizara ya uchukuzi tumechukua fedha nyingi sana za umma katika kuhakikisha reli ya kati inafanya kazi,” alisema.
Mwakyembe alisema ifikapo Septemba mwaka huu, karakana ya Morogoro itakuwa imeunda vichwa vinane, huku Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ikiagiza vichwa vya treni vitano.
Vichwa hivyo vya TPA vitatumika kwa ajili ya treni maalumu ya mizigo kwenda Kigoma na Mwanza, kuhudumia wafanyabiashara wa maeneo hayo na wa nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Uganda na Rwanda.
Utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwa TRL, umelenga kuiwezesha kampuni kiutendaji ili iweze kusafirisha tani milioni 3 ifikapo mwaka 2016 kutoka tani 200,000 zilizosafirishwa mwaka 2012 kupitia Reli ya Kati.

No comments:

Post a Comment