MOTO mkubwa umeteketeza gereza la Nyakiriba lililoko Magharibi mwa Rwanda, katika wilaya ya Rubavu, karibu na mpaka wa DRC.
Tukio hilo limeripotiwa kutokea Jumatatu (July 7) ambapo watu watatu wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 40 wamejeruhiwa vibaya kutokana na moto huo.
Akiongea na BBC, Mkuu wa wilaya ya Rubavu, Sheikh Hassan Bahame amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa waliopoteza maisha ni mahabusu watatu na kwamba majeruhi 44 walikimbizwa hospitali kuu ya wilaya kupata matibabu.
Amesema ilikuwa vigumu kwa jeshi la zima moto kutekeleza kazi yake ipasavyo kutokana na mazingira ya gereza hilo kuwa mlimani hali iliyopelekea vitu vingi kuteketea.
Mkuu huyo wa wilaya alieleza kuwa bado hawajafahamu chanzo na thamani ya vitu vilivyoteketea katika tukio hilo.
Tukio hili linatokea mwezi mmoja baada ya gereza jingine la Muhanga kuteketea kwa moto katika jimbo lililopo kusini mwa Rwanda.
Tayari uchunguzi umeanza juu ya matukio hayo yote mawili.
No comments:
Post a Comment