Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Yahaya Nawanda.
MKUU wa wilaya ya Iramba mkoa wa Singida,Yahaya Nawanda, ameahidi kuishi kwa siku tano katika nyumba za kabila la kisukuma kijiji cha Kizonzo tarafa ya Shelui, ili kuhakikisha zoezi la kukusanya michango ya ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho linafanikiwa.
Nawanda ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa uhamasishaji wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF),uliofanyika kwenye kijiji cha Kizonzo.
Alisema katika kipindi hicho atasimamia kwa karibu uchangiaji huo,ili ujenzi wa zahanati hiyo uweze kufanyika mapema iwezekanavyo.
“Ninyi ndugu zangu, mmekuwa mkipata taabu sana kufuata huduma ya afya kwenye zahanati ya kijiji cha Mgongo kwa kutembea umbali wa kilomita nane kwenda na kurudi. Akina mama wajawazito ndio wanaotaabika zaidi”, alifafanua Nawanda
“Sasa tunasema hatutakubali kabisa ninyi muendelee kutaabika kufuata matibabu umbali mrefu kiasi hicho.Tunataka kipindi kifupi kijacho,matibabu muyapate hapa hapa kijijini kwenu”.
Kutokana na hali hiyo Nawanda amewataka wananchi kujiandaa mapema kwa zoezi hilo la uchangiaji wa ujenzi wa zahanati yao unaotarajiwa uanza mapema iwezekanavyo.
Kuhusu mfuko wa afya ya jamii (CHF),mkuu huyo wa wilaya,alisema suala la kujiunga na mfuko huo ni la lazima kwa madai kwamba afya bora ni mtaji wa mwili wa binadamu ye yote.
“Wilaya yetu ya Iramba, ni wilaya ya kwanza nchini kwa vituo vyake vyote vya afya kuwa na dawa za kutosha wakati wote.Kwa hiyo mwanachama wa CHF, nawahakikishia kuwa mtapata tiba wakati wote pindi watakapougua”,alisema DC huyo.
Kwa mujibu wa Dc Nawanda, kuku moja wa kienyeji mwenye thamani ya shilingi 10,000 tu, anatosha kugharamia ada ya kaya moja yenye mume, mke moja na watoto wanane, kupata matibabu kwa kipindi cha mwaka moja bila kuongeza kiasi kingine cha fedha.
No comments:
Post a Comment