Sunday, June 29, 2014

WENGI WASHTUSHWA NA LINALOENDELEA KATIKA NDOA YA FLORA MBASHA, SOMA HAPA KUJUA MENGI!!!

HAKUNA neno zuri la kusema zaidi ya Mungu mkubwa! Ule mtafaruku ndani ya ndoa ya mwimba Injili mahiri Bongo, Flora na mumewe, Emmanuel Mbasha umedaiwa kumalizika kwa wawili hao kupatana, Risasi Jumamosi linakuwa nambari wani kukuhabarisha.
Kwa mujibu wa chanzo cha uhakika, wawili hao walikalishwa kikao cha upatanishi mapema wiki hii kilichokuwa chini ya familia.
Mume wa Flora Mbasha, Bw. Emmanuel Mbasha.

MANENO YA CHANZO
“Kikao cha familia kilikaa, Mbasha aliitwa akafika, Flora naye aliitwa akatokea, mazungumzo yalikuwa marefu lakini kimsingi waliamua kuweka kando mtafaruku wao na kuijenga upya ndoa yao,” kilisema chanzo.
Chanzo kiliongeza kuwa katika kikao hicho cha mwanzoni mwa wiki hii, miongoni mwa adidu za rejea ilikuwa kutokumbushia vikao vilivyopita ambapo hakukupatikana muafaka.

VIKAO VILIVYOPITA
Katika vikao vilivyopita, wahusika wakuu walikuwa wazazi wa Mbasha (mzee Maneno Mbasha, Zulfa Maneno), ndugu wa Flora na Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
Mwimbaji Injili mahiri Bongo, Flora Mbasha.

VIKAO VYA BAADAYE
Kwa mujibu wa chanzo, vikao vilivyofuata, wawili hao wakawa tayari kila mmoja ametema nyongo yake pembeni na kufikia makubaliano kwamba, ndoa yao isimame tena wakitumia maandiko kwenye Biblia kutoka kitabu cha Waebrania yanayosema: Ndoa na iheshimiwe na watu wote na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.

WAKORINTHO YAFUNGA KAZI
Kwa mujibu wa chanzo hicho, maneno mengine ya Biblia yaliyotumika kwenye kikao hicho mpaka wawili hao wakaamua kurudiana ni 1 Wakorintho 7:1-10 ambapo maandiko yanasema:
Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe na kila mwanamke awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake.
Flora Mbasha akiwa kwenye picha ya pamoja na mumewe, Emmanuel Mbasha.
Mke hana amri juu ya mwili wake bali mumewe vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake bali mkewe. Msinyimane, isipokuwa mmepatana kwa muda ili mpate faragha kwa kusali, mkajiane tena shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.
Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza, wala hapo si mimi, ila Bwana (Mungu), mke asiachane na mumewe, lakini ikiwa ameachana naye na akae asiolewe au apatane na mumewe, tena mume asimwache mkewe.

KIKAO CHA JUMAMOSI KUMALIZIA
Chanzo kilisema kuwa, kikao cha mwisho ambacho kitamalizia kuweka mambo sawa ili wawili hao waanze ngwe ya pili ya ndoa yao ambayo inaaminika itakuwa ya mwisho mpaka kifo kiwatenganishe, kinatarajiwa kufanyika leo jijini Dar es Salaam mahali ambapo hapakutajwa.
Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

MWANASHERIA ATAJWA
Mwanasheria wa Flora aliyejulikana kwa jina moja la Ado ametajwa kusimamia kikao hicho ili wawili hao waanze maisha mapya baada ya safari fupi ya mvurugano uliowafanya kuwa mbalimbali.

AONGEA NA RISASI JUMAMOSI
Juzi, Risasi Jumamosi lilimsaka mwanasheria huyo kwa njia ya simu yake ya mkononi ili kumsikia anasemaje kuhusu kutajwa kwenye usuluhishi wa ndoa hiyo ambapo alipopatikana alisema:
“Niko Arusha, Ijumaa nitarudi Dar. Kuhusu kikao cha usuluhishi siwezi kukwambia lakini suala la kuwapatanisha nalifahamu, nawaomba na ninyi msaidie kufanikisha jambo hilo zuri.”

VIPI KUHUSU KESI YA MADAI YA KUBAKA?
Hata hivyo, Wakili Ado hakutaka kugusia kuhusu kesi ya Mbasha iliyopo Mahakama ya Wilaya ya Ilala ambapo anadaiwa kumbaka shemejiye mara mbili (jina tunalo) ambayo kwa mujibu wa mahakama, upelelezi umekamilika na itasikilizwa Julai 17, mwaka huu.

KWA UPANDE WAKE FLORA
Risasi Jumamosi lilimwendea hewani, Flora ili kumsikia anasemaje kuhusu kuwepo kwa upatanishi kati yake na mumewe, Emmanuel.
Huyu hapa: “Ongea na wakili wangu atakwambia kila kitu.” Ambapo majibu ya wakili yalikuwa: ”Ninachojua mimi ni kwamba Flora ameshamsamehe mumewe na yuko tayari kuanza ukurasa mpya.”

MBASHA SASA
Kwa upande wake, Mbasha alipozungumza na gazeti hili juzi alisema kurejea upya kwa ndoa yake ni jambo la kuupendeza moyo wake.
“Mimi sina neno nipo tayari, nimeshasamehe yaliyotokea, Flora ni mke wangu jamani, nampenda sana kutoka moyoni.”

No comments:

Post a Comment