Friday, June 27, 2014

MFANYAKAZI WA TIGO AKUTWA AMEJINYONGA KWA KAMBA YA VIATU SHINGONI BAFUNI

MFANYAKAZI wa Kampuni ya simu ya Tigo, (MIC T Ltd.),  jijini Arusha, Mwita Makore, amekutwa amekufa nyumbani kwake maeneo ya Kimandolu huku akiwa na kamba za viatu shingoni kuashiria kwamba alijinyonga nazo kwa kujitundika kwenye bomba la bafuni kwake.

Hali hiyo imezua gumzo miongoni mwa wakazi wa jiji la Arusha wakihoji inawezekanaje mtu kujinyonga kwa kamba ya viatu hadi kufa huku wengine wakihoji uwezekano wa mwili wa mtu mzima kuning’inia kwenye bomba la bafuni.

Habari kutoka eneo la tukio zinadai kuwa mwili wa Makore ambaye alikuwa kitengo cha ‘store’, ulibainika Juni 20, mwaka huu baada ya kutoonekana wala kupatikana kwa simu zake za kiganjani kwa siku mbili mfululizo, hali iliyowalazimu wafanyakazi wenzake kwenda kumtafuta nyumbani kwake na kubaini kifo chake.

Mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo jijini humo aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake, alisema mara ya mwisho Makore kuingia ofisini ilikuwa ni Juni 18, mwaka huu.

“Unajua yeye kazi yake haimlazimu kuwa ofisini muda wote, hivyo akishamalizana na wateja wake huondoka, hivyo siku ya Alhamisi hakuja kabisa ofisini, lakini hakuna aliyekuwa na wazo kama kakutwa na jambo baya.

“Alikuja mteja anayehitaji vocha, ikabidi apigiwe simu, simu ikawa inaita haipokelewi, siku inayofuata wakaja wateja wengine, Mwita akapigiwa simu zake zikawa zinaita tu lakini hazipokelewi.

“Yule mteja akachukia akaamua kupiga simu makao makuu kueleza usumbufu anaoupata, ndipo nao wakawapigia viongozi hapa wakawaeleza kama hapokei simu kwanini wasimfuatilie nyumbani kwake pengine amepata matatizo,” alisema mfanyakazi huyo.

Alisema kuwa walipofika nyumbani kwake walikuta gari ya Kampuni ya Tigo ikiwa imeegeshwa vizuri, lakini funguo zake ziko ndani na milango imerejeshewa tu huku kwenye mlango wa kuingia ndani kwa Makore kukiwa na viatu vyake na walipopiga simu zake, wakasikia zikiita kutoka ndani ndipo wakaamua kuingia ndani.

“Tulipoingia pale mezani tulikuta kuna chupa ya soda, na simu zake tatu pamoja na kadi zake za benki, tukaendelea kuangalia maeneo mbalimbali ya nyumba hiyo ndipo tukamkuta Makore bafuni na kamba ya viatu shingoni,” alisema mfanyakazi huyo wa Tigo.

Mwananchi mwingine anayeishi maeneo ya Kimandolu, alisema tukio hilo limewashangaza sana kwani Makore alikuwa kijana mtaratibu asiye na makuu na alikuwa mpenzi wa mchezo wa pool table.

Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa kifo hicho alichodai ni cha kawaida kwani amekutwa amekufa nyumbani kwake na hakuna mahali palipovunjwa.

“Achana na habari za barabarani, amekutwa amekufa nyumbani kwake, hakuna mahali pamevunjwa, hiyo ni ‘natural death’,” alisema Sabas 

No comments:

Post a Comment