KIKOSI Kazi cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, kimebaini njia mpya ya wasafirishaji, ambapo sasa wanapitisha nchi jirani ili wasigundulike kirahisi na baadaye huzifuata.
Njia wanazotumia wasafirishaji hao ni kupitisha mizigo yao kwenye miji ya Maputo, Kampala na Nairobi.
Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya, Kamanda Godfrey Nzowa alisema wasafirishaji hao huagiza dawa hizo kutoka sehemu mbalimbali na kuzipeleka kwenye nchi ambazo hazina sheria kali.
Wamegundua kuwa Tanzania kuna sheria kali hivi sasa, wanashindwa kupitisha na kuamua kuzipitisha sehemu yenye sheria dhaifu
alisema.
Alisema kwa hali hiyo, sasa wasafirishaji wa dawa hizo wanaharibu njia za kawaida za ndege.
Kama ndege ilikuwa inatoka Pakistan na ilitakiwa itue nchini, haitafanya hivyo na badala yake itakwenda sehemu ambayo wamelenga kushusha mzigo huo
alisema.
Alisema kuanzia Januari hadi Mei mwaka huu, wamekamata kilo 250 za dawa za kulevya aina ya heroine na kilo tisa za cocaine na watuhumiwa 22 kufikishwa mahakamani.
Alisema watuhumiwa 16 kati ya hao ni raia wa kigeni na wanne kutoka nchini, ambao walikamatwa na dawa zenye thamani kubwa.
Watuhumiwa waliokamatwa na dawa zenye thamani zaidi ya Sh10 milioni, kesi zao zitasikilizwa Mahakama Kuu. Raia wa kigeni waliokamatwa na dawa za kulevya, Liberia (4), Palestina (4), Kenya (1), Nigeria (1), Marekani (1) na Iran (8).
No comments:
Post a Comment