Na Hilali Ruhundwa
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida binti mmoja mkazi wa kitongoji Kemitoma kijiji Mwemage kata ya Kilimilile wilaya ya Missenyi mkoani Kagera, amemlisha mama yake mzazi kinyesi na mkojo vya binadamu.
Binti huyo aliyekiri kufanya kitendo hicho cha kinyama, anatambulika kwa jina la Imelda Kasente mwenye umri wa kati ya miaka 33 na 35 ambaye anaishi na mama yake mzazi mwenye umri wa miaka 85 (jina linahifadhiwa) anadaiwa kumfanyia mama yake vitendo hivyo vya kikatili kwa muda sasa ili akitumie kama chakula.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho Bi. Jeneroza Blasio amethibitisha kufahamu tukio hilo na kusema kuwa bibi kizee huyo amekuwa akilalamika kulishwa kinyesi na kunyweshwa mkojo vya binadamu na mtoto wake wa kumzaa.
Binti huyo alipoulizwa sababu ya kumfanyia vitendo hivyo mama yake mzazi, (kwa kigugumizi) amekana kutenda vitendo hivyo. “Mama yangu huwa ananitesa kumtunza. Nilimwambia ajifulie nguo akakataa eti hana nguvu nikamwambia nimchimbie kashimo nje ya nyumba ajisaidie akasema hana nguvu za kumfikisha nje”. Amesema Imelda na kuongeza, “Nilikiri kosa mbele ya watu wakanipa adhabu ya kumbeba mgongoni mama yangu na kuzunguka naye”.
Akizungumza kwa masikitiko na uchungu, bibi huyo amesema kuwa hana nguvu za kujisitiri mwenyewe na alitegemea mtoto wake kumtunza lakini hali si kama alivyotegemea. “Mtoto wangu wa kumzaa alinilisha kinyesi na kuninywesha mkojo na kunilazimisha nivimeze. Nililazimika kuvimeza kwa kuwa sikuwa na jinsi”. Amesema bibi huyo.
Balozi nyumba kumi wa eneo hilo Bwana Victor Andrea ameiambia Radio Karagwe kuwa bibi huyo alimkimbilia na kumweleza kuwa analishwa kinyesi na mkojo na binti yake. “Bibi huyo alikuja kunieleza kuhusiana na kulishwa kinyesi na mkojo nikasikitika sana na sasa tuna mkutano wa kutoa adhabu kali kwa binti huyo. Adhabu ya awali ilikuwa kumbeba mama yake lakini haitoshi na sasa ninavyoongea nawe leo hii tuna kikao cha kujadili jambo hilo”. Amesema bwana Andrea.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Radio Karagwe kupitia kipindi cha Habari Nyepesi, wamelaani kitendo hicho na kuiomba serikali na jamii kupiga vita vitendo vya unyanyasaji kwa wazee.
Vitendo vya unyanyasaji kwa wazee mkoani Kagera vimekuwa sugu na wazee wameendelea kunyanyasika bila msaada wowote. Jeshi la polisi mkoani Kagera linasema kuwa linachukulia wazee kama watu wengine na siyo kama kundi maalum.
No comments:
Post a Comment