Thursday, April 3, 2014

MAMA SALMA KIKWETE AKABIDHIWA CHETI CHA ULEZI WA HIYARI WA CHAMA CHA WENZA WA MABALOZI WA AFRIKA WAISHIO UBELGIJI

 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipokea cheti maalum cha ulezi wa heshima wa Chama cha wenza wa mabalozi wa nchi za Afrika walioko nchini Ubelgiji  (Honory Patronese of the Association of the Spouses of African Ambassadors in Belgium) kutoka kwa Mke wa Balozi wa Cameroon nchini Ubelgiji Mama Christiane Eloundov de Evina  wakati wa chakula cha mchana walichowaandalia wake wa Marais wa Afrika jijini Brussels tarehe 2.4.2014
Mke wa Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mama Adelaida Kamala akimkabidhi Cheti Maalum  cha ulezi wa heshima cha wenza wa mabalozi wa Afrika walioko Ubelgiji, Mke wa Rais wa Cameroon Mama Chantal Biya wakati wa chakula cha mchana walichowaandalia wageni hao kwenye hoteli ya Sheraton.
************************************

Na Anna Nkinda – Brussels, Ubelgiji
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amepewa cheti na Umoja wa wake wa Mabalozi  wa Afrika waishio katika  nchi za Jumuia ya  Ulaya kwa kutambua na kuthamini mchango wake na kazi anazozifanya za kuwasaidia wanawake, wasichana  na watoto wa Tanzania. 
Cheti hicho amekabidhiwa jana katika hafla fupi  ya chakula cha mchana kilichoandaliwa na wake hao wa mabalozi katika ukumbi wa mikutano uliopo Hoteli ya Sheraton mjini Brussels.

Mama Kikwete ni mmoja kati ya wake wa Marais wa tano wa  Afrika waliokabidhiwa vyeti hivyo vya heshima kutokana na kazi zao wanazozifanya za kuisaidia jamii na kuhakikisha kuwa inapata mahitaji ya muhimu kama huduma ya afya na elimu.
Akiongea kabla ya kuwakabidhi wake hao wa marais vyeti hivyo Mke wa Balozi wa Equatorial  Guinea  ambaye pia ni rais wa umoja huo Mama Mangue de Nvono Nca alisema nia ya kuanzishwa kwa umoja wao ni kulitambulisha bara la Afrika ambalo linajulikana  kuwa na  changamoto za njaa, magonjwa, kutokuwa na haki na  usalama wa kutosha katika nchi za Ulaya.
“Siyo kama Bara letu la Afrika linakabiliwa na changamoto peke yake bali pia limejaliwa kuwa na  umoja, mshikamano na  ukarimu na haya yote yamejidhihirisha  kwetu leo hii kutokana na kitendo cha wake wa marais wetu kushiriki pamoja nasi katika hafla hii  na kubadilishana mawazo”, alisema Mangue de Nvono Nca. 
Alisema umoja huo  unatambua kazi kubwa inayofanywa na wake wa Marais wa Afrika kwa jinsi wanavyowaunga mkono wenza wao kwa  kufanya kazi   ambazo malengo yake makubwa ni  kuwasaidia wanawake, wasichana , watoto na watu ambao wako katika makundi  hatarishi ndani ya jamii. 

Akiongea  kwa niaba ya wenzake mara baada ya kutunukiwa vyeti hivyo Mke wa Rais wa Congo Brazzavile Mama Antoinette N’Guesso  aliwashukuru wake hao wa mabalozi kwa kazi wanayoifanya ya kulitangaza bara la Afrika kuwa ni nchi ya umoja, mshikamano na ukarimu jambo ambalo litaondoa dhana iliyopo miongoni mwa watu kuwa kitu pekee kilichopo barani Afrika ni matatizo.
Wengine waliokabidhiwa vyeti hivyo ni pamoja na  Malkia wa  Swaziland Inkhosikati Zena Seraya Mahlangu , Mke wa Rais wa Madagascar Mama Lalao Rajaonarimampianina, Congo Brazzaville  Mama Antoinette N’Guesso  na  Cameroon  Mama Chantal Biy.
Wake hao wa Marais wameambatana na wenza wao ambao ni Marais wa Afrika wanaohudhuria mkutano wa nne  wa wakuu wa nchi za Afrika na Jumuia ya Ulaya unaofanyika nchini humo.
 Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Mke wake Mama Salma akipokewa  na ujumbe wa Tanzania unaohudhuria mkutano wa siku mbili baina ya Afrika na Ulaya mara baada ya kuwasili kwenye Hoteli ya Sheraton huko Brussels  nchini Ubelgiji akitokea nchini Uingereza.
 Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Mke wake Mama Salma akipokewa  na ujumbe wa Tanzania unaohudhuria mkutano wa siku mbili baina ya Afrika na Ulaya mara baada ya kuwasili kwenye Hoteli ya Sheraton huko Brussels  nchini Ubelgiji akitokea nchini Uingereza.
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na wenza wa mabalozi wa nchi za Afrika wanaowakilisha nchi zao nchini Ubelgiji. 
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisalimiana na Mke wa Rais wa Madagascar Mama Lalao Rajaonarimampianina muda mfupi kabla ya kushiriki kwenye chakula cha mchana kilichoandaliwa na wenza wa mabalozi wa Afrika kwa ajili ya wake wa Marais na Wakuu wa nchi za Afrika wanaohudhuria mkutano wa Afrika na Ulaya unaofanyika huko Brussels.
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisalimiana na baadaye wakibadiishana mawazo na Mke wa Rais wa Congo Mama Antoinnethe Sassou Nguesso wakati wa hafla ya chakula cha mchana walichoandaliwa na Jumuia ya wenza wa mabalozi wa Afrika wanaowakilisha nchi zao huko Ubelgiji.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na wake wa Marais na Wakuu wa nchi za Afrika pamoja wa wenza wa Mabalozi wa nchi hizo mara baada ya kupata chakula cha mchana kilichoandaliwa na wenza hao. 
Picha na John Lukuwi

No comments:

Post a Comment