Monday, April 28, 2014

KIBADENI AKERWA NA UZEMBE WA WACHEZAJI LIGI KUU

Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KOCHA mkongwe na mchezaji machachari wa zamani wa Simba na timu ya taifa ya Tanzania na sasa Ashanti United, Abdallah King Kibadeni `King Mputa` amesema kwa uzoefu wake anafahamu kuwa vijana wengi wanashindwa kujitambua na kujitathimini.
Akihojiana na mtandao huu, Kibadeni amefafanua kuwa wapo vijana katika Nyanja mbalimbali za michezo na burudani mfano bongo fleva, filamu, mpira na vinginevyo, lakini kwa wachezaji wa soka kujitambua imekuwa shida sana.
“Ukiangalia vijana wanaofanya Bongo fleva , siasa, wengi wao wanatambua kuwa muziki na siasa ni kazi yao na wanaweza kupata maisha mazuri kwa kazi hizo”.
“Ukija kwa vijana wetu wa mpira, huwa wanaridhika mapema na wanacheza kwa sifa”.
“Akicheza kwa mafanikio na wakamsifia basi inakua shida kwa walimu”.
“Unapomchukua na kumuweka kambini ili umtulize, bado anashindwa kujitambua. Kambini kuna uwanja, walimu na kila kitu, lakini hata kuamka inakuwa shida”.
“Wanataka mwalimu awasimamie, awasukume, sasa unaanzaje kusema wachezaji hawa wanajitambua”. Alisema Kibadeni.
Kibadeni aliwaomba walimu wenzake kuwaelemisha vijana kwasababu wanachukua nafasi ya wazazi.
“Tanzania tuko milioni ngapi? Kijana anapochaguliwa miongoni mwa watanzania wengi wanaocheza soka lazima aheshimu jambo hilo”.
“Leo hii timu ya taifa inakuwa na wachezaji 30, hivi kuna watu wangapi wanaocheza mpira Tanzania?, hawa vijana lazima waelimishwe ili wajitambue na kutathimini malengo yao”. Alisema Kibadeni.
Kibadeni aliongeza kuwa vijana lazima watambue kuwa makocha wao ni wazazi hivyo ni haki yao kuuliza wanakula nini, wanalala wapi na wanatumiaje pesa zao.
“Kijana ukimfuatilia na fedha zake anaona kama unamuonea. Kocha ni mzazi na lazima ajue unachokipata anafanyia nini kwa maisha ya baadaye”.
“Hatuna malengo ya kuwabana na hela zao, lakini ni muhimu kuwaeleza ukweli kuwa wanachokipa leo kinaweza kisipatikane kesho”.
“Mpira una muda wake, leo utaonekana mzuri kesho utaoekana hufai. Lazima ujitambue na kujua utaishi vipi baadaye. Sasa kwa kuzingatie hili, kwanini makocha tusikufuatilie?” Alihoji Kibadeni.
“Lazima wajipangia malengo yao. Lazima wajue wanataka kucheza kwa muda gani na baada ya hapo wawe nani?, wanataka kuwa mameneja, makocha au viongozi”.
“Vijana wasipokuwa na malengo watajikuta wanacheza kwa mwaka mmoja halafu wanapotea kabisa”.
“Wawe na nidhamu na wajijue wanacheza kwa ajili ya nani, kwa ajili ya nchi au klabu”.
“Lazima tuwe na wivu, kwani tumekatazwa kuwa wachezaji bora wa dunia au Afrika?”.
“kwanini watu bora waonekana wanatoka magharibi?, lazima vijana wetu wawe wapambanaji na kuwa na malengo ya mbali”. Alihitimisha Kibadeni.

No comments:

Post a Comment