Vyombo vya usalama nchini Yemen vimetaarifu kuwa zaidi ya wahamiaji arobaini wenye asili ya Afrika wamezama baharini, baada ya mashua walimokuwa wakisafiria kuzama katika pwani ya kusini mwa nchi hiyo.
Manuwari ya jeshi la Yemen ambalo lilikuwa katika eneo hilo, imefanikiwa kuwaokoa wahamiaji wengine wapatao thelathini.
Wizara ya ulinzi nchini Yemen imesema kuwa mashua hiyo iliyokuwa ikisafirisha wahamiaji haramu, ilizama katika mkoa wa Kusini wa Shabwa, eneo ambako maelfu ya wahamiaji wa Kiafrika huwasili kila mwaka.
Kwa mujibu wa shirika la Kimataifa la Uhamiaji la IOM, wengi wa wakimbizi wanaojaribu kuvuka guba ya Eden wanatoka Somalia na Ethiopia.
Pia shirika hilo limeongeza kuwa wahamiaji hao hufanya safari ndefu na hatari ili kukwepa umasikini, unyanyazaji au vita katika mataifa yao.
Wahamiaji hao baada ya kuwasili Yemen, wengi wao hutaraji kupata kazi nchini Saudi Arabia na mataifa ya Guba, lakini mamia ya wahamiaji wa Kiafrika hufa kila mwaka wakijaribu kuvuka eneo hilo la Guba wakitafuta maisha bora katika mataifa yaliyoendelea.
No comments:
Post a Comment