Friday, March 7, 2014

JE NI WAZO ZURI: UKIVAA NUSU UCHI NA MILEGEZO UCHAPWE BAKORA HADHARANI??



JAMBO hili limeanzia huko jijini Arusha, jiji lenye mchanganyiko mkubwa wa tamaduni mbalimbali, ikiwa ni kati ya miji iliyobarikiwa kuwa na vivutio vingi vya kitalii na hali nzuri nzuri ya hewa hivyo kuwavutia wageni wengi kutoka nchi za nje kuja kutembea jijini humo.

Licha ya kuwa na mchanganyiko mkubwa wa watu na tamaduni mbalimbali jijini Arusha kumekuwako na baadhi ya vitendo ambavyo karibu maeneo mengi nchini Tanzania hasa mijini vinajitokeza, kama vile kuvaa mavazi yanayoweka baadhi ya maeneo yao ya mwili yakiwa wazi lakini pia kwa vijana wa kiume wanavaa milegezo.

Jambo hilo limepingwa vikali na wananchi wa Kijiji cha Olgilai, wilayani Arumeru jijini Arusha ambapo uongozi wa kijiji hicho umekubaliana na wananchi hao, kutoa adhabu ya  kuwachapa viboko hadharani wanawake watakaovaa mavazi ya nusu uchi hasa vimini na vijana wa kiume wanaovaa suruali chini ya makalio (milegezo).

Mwenyekiti wa Kijiji cha Olgilai, Godson Boazi katika barua yake ya Januari 24, mwaka huu kwa viongozi wa makanisa kijijini hapo, aliwaomba kuunga mkono hatua hiyo katika kurekebisha tabia ndani ya jamii yao.

“Viongozi wa dini tunafahamu kazi kubwa ya kutunza kundi la Mungu likae kwenye maadili mema. Hivyo basi tunaomba mtusaidie jukumu hili ambalo tumeambatanisha kwenu kwa barua,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo inaendelea kueleza: “Vijana wa kiume wanaovaa mlegezo, uendeshaji ovyo wa pikipiki, wavuta bangi, watumiaji wa madawa ya kulevya, wanywa gongo na viroba, uchezaji kamari na karata. Wanaotukana ovyo barabarani na kupiga kelele za uvunjaji wa amani, wezi wa vitu vikubwa na vidogo kama kuku, ndizi, viazi, mahindi na mboga mashambani watashughulikiwa.”

Chanzo cha habari hii kinaripoti kuwa wanakijiji wote wamefurahishwa na kitendo hicho ambapo kwa kauli moja wamepitisha azimio hilo ili kujenga kijiji chenye nidhamu na amani tofauti na hali ilivyo sasa.

Watanzania tupo hapo???
Chanzo: Malunde blog


No comments:

Post a Comment