Monday, March 31, 2014

DC KAHAMA ALIAGIZA JESHI LA POLISI KUMSAKA MTENDAJI WA KATA ALIYETOROSHA MKULIMA WA BANGI

Baadhi ya miche ya bangi iliyopatikana katika shamba hilo ikiwa imeshikiliwa na askari polisi
Mkuu wa wilaya ya Kahama Benson Mpesya (kulia) akitoa agizo hilo kwa mkuu wa kituo cha polisi Kahama Elias Haway na mkuu wa Upelelezi Wilaya Twaha Juma.
MKUU wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Benson Mpesya, ameliagiza jeshi la polisi wilayani humo kumtafuta na kumkamata Afisa Mtendaji wa Kata ya Mega, Peter Kupingwa, kwa tuhuma za kuhusika katika kumtorosha mkulima wa Bangi.

Mpesya ametoa agizo hilo jana baada ya kufika katika shamba lililokuwa limelimwa bangi hiyo lililopo katika kijiji cha Masabi, huku akiwa ameongozana na askari polisi na kukuta bangi hiyo imeshavunwa na kubaki miche kadhaa iliyochukuliwa kama ushahidi. 
Imedaiwa Afisa mtendaji huyo alitoa agizo la kuachiwa kwa Mtuhumiwa Juma Maliatabu ambaye juzi alikamatwa na sungusungu baada ya Afisa Kilimo wa kata hiyo Edwin Kasaba kuwapa taarifa za kukuta zao hilo katika shamba la Malingita.

Mpesya ametaka kukamatwa kwa Kupingwa ambaye ni mwajiri wake kutokana ma kuonesha kukerwa na kitendo alichokifanya cha kutetea na kuendelea kuwakumbatia watuhumiwa na kuongeza kuwa hakuna aliye juu ya sheria.
Shamba hilo la Hekari moja na nusu limelimwa mahindi huku yakiwa yamechanganywa na zao la Bangi ndani yake, jambo lililomfanya Afisa kilimo kwenda kukagua kama sehemu yake ya kazi kutembelea mashamba ya wakulima na kutoa ushauri.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, Shamba hilo linamilikiwa na Ndugu wawili Juma Maliatabu na Malingita Maliatabu ambaye pia hadi sasa hajulikani alipo baada ya kukosekana katika msako huo wa Polisi ambao bado unaendelea. 
Hata hivyo Jeshi la wilaya ya Kahama lililokuwa likiongozwa na Mkuu wa kituo cha polisi Kahama Elias Haway na Mkuu wa Upelelezi Wilaya Twaha Juma limefika katika kaya za Watuhumiwa kwa lengo la kuwakamata bila Mafanikio.

No comments:

Post a Comment