Gari
aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T.589 AZS likiwa limebeba
magunia ya madawa ya kulevya aina ya bhangi mara baada ya kukamatwa
eneo la Sanawari jijini Arusha na askari wa kitengo cha kuzuia Madawa ya
Kulevya mkoani hapa. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi
Arusha)
………………………
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
JESHI
la Polisi Mkoani Arusha limewakamata watu watano wakiwa na magunia
saba ya madawa ya kulevya aina ya bhangi wakiwemo mke na mume. Awali
askari wa Kitengo cha Kuzuia Madawa ya Kulevya Mkoani hapa wakiwa doria
walipata taarifa toka kwa raia wema iliyoeleza kuwepo kwa watu
wanaosafirisha madawa hayo.
Mara
baada ya kupata taarifa hiyo askari hao waliweka mtego maeneo ya
Sanawari ambapo muda wa saa 3:30 usiku walifanikiwa kuwakamata
watuhumiwa wawili ambao ni Hussein Rashid (35) mkazi wa Sakina, dereva
pamoja na mwenzake Sebastian Wilbert (37) Fundi magari, mkazi wa Ilboru
wakiwa wanasafirisha magunia matano ya madawa ya kulevya aina ya bhangi
yenye uzito wa kilogramu 171 kuelekea nchi jirani ya Kenya kwa kutumia
gari aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T. 589 AZS.
Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas alisema kwamba,
mara baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa walikiri kosa hilo na kumtaja
mwanamke aitwaye Flora John (38) Mkazi wa Ekenywa- Ngaramtoni kuwa ndio
aliyewauzia.
Kamanda
Sabas aliendelea kwa kusema kwamba, askari hao walianza kumfutilia
mwanamke huyo ambapo jana Jumanne tarehe 05.08.2014 walikwenda nyumbani
kwake na kumkuta mtuhumiwa ambaye ni muuzaji akiwa na mume wake aitwaye
John Meleji (45) Mkazi wa Ekenywa na mara baada ya kufanya upekuzi
walikuta gunia moja la madawa ya kulevya aina bhangi ndani ya nyumba
hiyo.
Mbali
na kuwakamata watuhumiwa hao ambao ni mke na mume pia askari hao
walimkamata jirani yao aitwaye Loseriani Metelami (21) Mkulima mkazi wa
Ekenywa baada ya yeye pia kukutwa na gunia moja la madawa ya kulevya
aina ya bhangi hivyo kufanya jumla ya magunia yaliyokamatwa kuwa saba.
Watuhumiwa hao watano wanatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi karibuni mara baada ya upelelezi kukamilika.
0 comments:
Post a Comment